MAPYA YAANZA KUIBUKA UVAMIZI WA WESTGATE
Nairobi. Picha zilizonaswa kupitia kamera za
CCTV zilizofungwa kwenye jengo la kibiashara la Westgate Mall mjini
Nairobi zinaonyesha kwamba magaidi waliovamia jengo hilo walikuwa wanne,
hivyo kuanza kuibua mtizamo mpya kuhusu magaidi waliovamia jengo hilo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, taarifa
hizo ambazo bado si rasmi kutoka kwa mmoja wa maofisa wa juu wa Serikali
ya Kenya juzi, zilieleza kwamba watu wanne wakiwa na silaha za kisasa
ndio walioonekana kupitia kamera hizo za siri, hivyo kuanza kuwepo kwa
uwezekano wa kupungua kwa idadi ya awali ya watuhumiwa hao wa ugaidi
waliovamia jengo hilo
.
.
Awali, Serikali ya Kenya ilieleza kwamba wavamizi
hao ambao walijitambulisha kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la Al
Shabaab la Somalia waliotekeleza uvamizi huo Septemba 21, walikuwa kati
ya 10 hadi 15 na kusababisha vifo vya watu 67, idadi ambayo imeanza
kutiliwa walakini.
Kati ya waliouawa, kwa mujibu wa taarifa za
Serikali, walikuwemo wanausalama sita, watatu wakiwa maofisa usalama wa
jeshi na watatu wakiwa maofisa usalama wa polisi ambao waliuawa kwati wa
kujibizana risasi walipokuwa wakijaribu kuwadhibiti wavamizi hao.
Taarifa hizi zimeanza kuvuja wakati wataalamu wa
masalia ya miili ya binadamu wakiendelea kufanya uchunguzi kwenye mabaki
ya miili ya watu waliokuwa wamenasa kwenye vifusi vya jengo hilo.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea, tayari vijana
kadhaa wameshakamatwa kwenye eneo la watu wa makazi duni la majengo
mjini Nairobi, kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano kama sehemu ya polisi
kujaribu kuwanasa wavamizi hao ambao kwa mujibu wa taarifa za awali,
walifanikiwa kutoroka kupitia mtaro wa maji machafu unaotoka kwenye
jengo hilo.



Post a Comment: