Wabunge Kenya wakosa kupitisha mswada wa jinsia
![]() |
| Rais wa Kenya: Uhuru Kenyatta |
Wabunge nchini Kenya wanatarajiwa kupiga kura, kwa mara nyingine, ya kupitisha ama kupinga mswada wa sheria kuhusu usawa wa jinsia katika nyadhifa za uteuzi na siasa.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Kenya, nyadhifa zote za uteuzi na uchaguzi katika
afisi za umma hazifai kuchukuliwa na zaidi ya theluthi mbili ya jinsia
moja, iwe wanawake ama wanaume.
Mswada huo ulihitaji wabunge
kuungwa mkono na wabunge 233 ndipo uidhinishwe lakini idadi ya wabunge
waliohudhuria kikao, yenyewe haikufikia kiwango hicho.
Baada ya kura kupigwa, wabunge 179 waliunga mkono mswada huo, 16 wakapinga na 5 wakakosa kutangaza msimamo wao.
Wiki
iliyopita mswada huo ulifeli ambapo ni wabunge 195 pekee waliouunga
mkono, 28 wakaupinga, wawili wakakosa kutangaza msimamo wao huku 24
wakikataa kupiga kura.
Mwenyekiti wa muungano wa wabunge wanawake
nchini Kenya Cecily Mbarire alikuwa awali ameeleza matumaini kwamba
mswada huo ungeidhinishwa lakini hilo halikuwa.
"Tuna matumaini
kuwa mswada huu utaptishwa hivi leo, tumekuwa tukizungumza na wenzetu
wanaume, na kuwarai kutuunga mkono, na tuna matumaini,” alisema awali.
Kura
ya leo ilipigwa siku ya mwisho kabla ya wabunge kwenda likizoni, na kwa
kawaida kikao kama hicho huhudhuriwa na wabunge wachache.
Wabunge wanatarajiwa kwenda likizo ya mwezi mmoja baada ya kikao cha leo alasiri.
Rais
Uhuru Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa muungano wa Jubilee, ulio na
wanachama wengi bungeni, alikuwa amewaomba wabunge kupitisha mswada huo.
![]() |
| Mh Raila Odinga |
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, wanawake hawakuchaguliwa katika nyadhifa za ugavana na useneta.
Kati ya wabunge 290 waliochaguliwa na wananchi mwaka 2013, asilimia 5.5 pekee ya wanawake ndio waliochaguliwa.
Kati ya wawakilishi wa wodi 1450, ni wanawake 88 pekee waliochaguliwa.
Bunge la kenya linajumuisha wabunge 290 waliochaguliwa na wananchi, wabunge 47 wanawake waliochaguliwa na wananchi kuwakilisha kaunti 47, na wabunge 12 maalum walioteuliwa na vyama vya kisiasa na spika wa bunge.


Post a Comment: